Joshua 1

Bwana Anamwagiza Yoshua

1 aBaada ya kifo cha Musa mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua mwana wa Nuni, msaidizi wa Musa: 2 b“Mtumishi wangu Musa amekufa. Sasa basi, wewe pamoja na watu wote hawa, jiandaeni kuvuka huu Mto Yordani kuingia nchi ambayo karibu nitawapa wana wa Israeli. 3 cKila mahali nyayo za miguu yenu zitakapokanyaga nimewapa, kama vile nilivyomwahidi Musa. 4 dNchi yenu itaenea kuanzia jangwa hili hadi Lebanoni, tena kuanzia mto mkubwa wa Frati, yaani nchi yote ya Wahiti, hadi Bahari ile Kubwa
Yaani Bahari ya Mediterania.
iliyoko upande wa magharibi.
5 fHakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.

6 g“Uwe hodari na shujaa, kwa sababu wewe ndiwe utakayewaongoza watu hawa kuirithi nchi niliyowaapia baba zao kuwapa. 7 hUwe hodari na uwe na ushujaa mwingi. Uwe na bidii kutii sheria yote aliyokupa Musa mtumishi wangu, usiiache kwa kugeuka kuelekea kuume au kushoto, ili upate kufanikiwa popote uendako. 8 iUsiache Kitabu hiki cha Torati kiondoke kinywani mwako; yatafakari maneno yake usiku na mchana, ili upate kuwa mwangalifu kufanya kila kitu sawasawa na yote yaliyoandikwa ndani yake. Ndipo utakapofanikiwa na kisha utastawi. 9 jJe, si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na shujaa. Usihofu wala usivunjike moyo, kwa kuwa Bwana Mwenyezi Mungu wako atakuwa pamoja nawe kokote uendako.”

10 kNdipo Yoshua akawaagiza maafisa wa watu akisema, 11 l“Pitieni katika kambi yote mkawaambie watu, ‘Wekeni tayari mahitaji yenu. Siku tatu kuanzia sasa mtavuka hii Yordani ili kuingia na kuimiliki nchi ambayo Bwana Mwenyezi Mungu wenu anawapa iwe yenu wenyewe.’ ”

12 mLakini kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, Yoshua akasema, 13 n“Kumbukeni agizo lile Musa mtumishi wa Bwana alilowapa: ‘Bwana Mwenyezi Mungu wenu anawapa ninyi raha, naye amewapa nchi hii.’ 14 oWake zenu, watoto wenu na mifugo yenu watakaa katika nchi ile Musa aliyowapa mashariki ya Yordani, lakini mashujaa wenu wote, wakiwa wamevikwa silaha kikamilifu lazima wavuke mbele ya ndugu zenu. Imewapasa kuwasaidia ndugu zenu hadi 15 p Bwana awape nao raha, kama alivyokwisha kufanya kwa ajili yenu hadi wao pia watakapokuwa wamemiliki nchi ile Bwana Mwenyezi Mungu wenu anayowapa. Baada ya hilo, mwaweza kurudi na kukalia nchi yenu wenyewe, ambayo Musa mtumishi wa Bwana aliwapa mashariki mwa Yordani kuelekea linakochomoza jua.”

16 qNdipo wakamjibu Yoshua, “Chochote ambacho umetuagiza tutafanya na popote utakapotutuma tutakwenda. 17 rKama vile tulivyomtii Musa kikamilifu, ndivyo tutakavyokutii wewe. Bwana Mwenyezi Mungu wako na awe pamoja nawe tu kama vile alivyokuwa pamoja na Musa. 18Yeyote atakayeasi neno lako na kuacha kuyatii maneno yako, au chochote utakachowaamuru, atauawa. Uwe imara na hodari tu!”
Copyright information for SwhKC